Usafiri wa reli katika mikoa ya kanda ya Ziwa ambao umesimama kwa takribani miaka
mitatu iliyopita,huenda ukarejea upya kuanzia mwezi Julai mwaka huu baada ya kuwasili kwa
vipuri vilivyoagizwa kutoka nje ya nchi kwa ajili ya kukarabati kichwa cha treni ya abiria namba 8818 iliyokuwa ikienda maeneo hayo ambayo imeharibika.
Hayo yameelezwa na Meneja wa Karakana kuu ya reli iliyopo Mkoani Morogoro, Mhandisi Ngoso Ngosomwile wakati wa ziara ya naibu waziri wa uchukuzi, Mh. Athumani Mfutakamba ambapo amesema tayari vipuri hivyo vimeagizwa tangu mwishoni mwa Desemba, na zoezi la kuvisuka upya huenda likachukua takribani miezi sita, wakati matengenezo yake yakitarajiwa kuchukua mwezi mmoja.
Amesema tayari serikali imewakabidhi fedha zilizotengwa kwaajili ya ukarabati na matengenezo ya injini na mabehewa ya treni pamoja na kuweka teknolojia mpya ya vifaa ndani ya mabehewa huku bado fedha zaidi ya shilingi bilioni 1.8 zikihitajika kwaajili ya matengenezo ya matengenezo ya mabehewa ya abiria.
Kwa upande wake naibu waziri wa uchukuzi Mhe. Mfutakamba ambaye ameeleza kushangazwa na uagizaji huo wa vipuri kuchukua muda mrefu, ametaka kuharakishwa kwa matengenezo hayo ili usafiri huo urejee upya kutokana na kuwa hitaji kubwa la wasafiri hasa na kwamba kusimama kwake kumeendelea kuisababishia hasara kubwa serikali.
Naibu waziri Mfutakamba, ameiagiza menejimenti ya shirika hilo kushirikiana kwa karibu na viwanda vya ndani ya nchi ikiwemo viwanda vya mang’ula na mzinga, kwa ajili utengenezaji wa vipuri ili kuokoa muda na fedha.
Usafiri kwa njia ya reli katika mikoa ya kanda ya ziwa, ulisitishwa na kampuni ya rites ya india iliyokuwa ikiendesha shirika la reli trl tangu mwaka 2009 hadi mwishoni mwa mwaka jana serikali ilipoamua kuvunja mkataba na kampuni hiyo kutokana na kukosekana kwa ufanisi katika uendeshaji wa shirika hilo.
No comments:
Post a Comment