Freeman Mbowe |
Upande wa mashtaka katika kesi inayowakabili Mwenyekiti wa Taifa wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake 18, utaongeza mashtaka matano zaidi na kufikia 13 badala ya manane ya awali na kesi hiyo itaanza kusikilizwa
mfululizo kuanzia Februari 22 hadi Machi 3, mwaka huu.
Mbali na Mbowe, vigogo wengine wanaokabiliwa na mashtaka ya kufanya maandamano Januari 5 mwaka juzi, ni Katibu Mkuu Dk. Wilbroad Slaa na mkewe Josephine Slaa, Mbunge wa Moshi Mjini, Filemon Ndesamburo na Mbunge wa Rombo, Joseph Selasini.
Wengine ni Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba na wenzao, wanatuhumiwa kufanya maandamano haramu.
Januari 5, mwaka jana, viongozi hao wanadaiwa kufanya maandamano ambayo hayakuruhusiwa na polisi, na hivyo kusababisha vurugu kubwa iliyopelekea polisi kuua watu watatu. Ilidaiwa kuwa maandamano hayo yalipangwa kwa lengo la kupinga kuchaguliwa kwa meya wa Halmashauri ya Jiji la Arusha, Gaudence Lyimo.
Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Arusha, Bw Charles Magesa, aliiahirisha kesi hiyo hadi Februari 21, baada ya kubaini kwamba baadhi ya washtakiwa hawakuwepo mahakamani hapo.
Baadhi ya watuhumiwa walitoa taarifa ya udhuru kupitia kwa wadhamini wao, lakini wengine hawakutoa taarifa kabisa hali ambayo ilimfanya Wakili anayewatetea Method Kimomogoro kuiomba mahakama watakapokuja katika tarehe iliyopangwa, wajieleze kwa nini hawakufika mahakamani na hatua zichukuliwe dhidi yao.
Washtakiwa ambao hawakufika mahakamani hapo lakini wadhamini wao walitoa taarifa ni Mbowe anayedhaminiwa na John Bayo, Dk. Slaa anayedhaminiwa na Gerald Emmanuel, Lema anayedhaminiwa na Elibariki Malley, na Selasini ambaye mdhamini hakufika na badala yake alimtuma mtu mwingine kutoa taarifa.
Wadhamini hao walisema washtakiwa walikwenda jijini Dar es Salaam, kuhudhuria shughuli ya kumuaga mbunge mwenzao Regia Mtema aliyefariki kwa ajali ya gari Jumamosi iliyopita.
Katika uamuzi wake, Hakimu Magesa alisema kisheria mdhamini anatakiwa kutoa taarifa mwenyewe lakini kwa vile baadhi walishindwa na wametoa taarifa japo kimsingi sio wao, itakuwa sio busara kukataa taarifa hizo.
No comments:
Post a Comment