Jan 16, 2012
MKUU WA MKOA DSM ASEMA BADO MISAADA INAHITAJIKA KWA WAHANGA WA MAFURIKO!!
NA MAGRETH KINABO – MAELEZO
16/1/2012
MKUU wa mkoa wa Dares Salaam Said Mecky Sadick amesema bado misaada zaidi inahitajika ili kuweza kuwasaidia wahanga wa mafuriko hususan ya shughuli za ujenzi na mahitaji ya watoto walioanza shule.
Kauli hiyo ilitolewa leo (jana) na Sadick wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisi kwake jijini Dares Salaam mara baada ya kupokea msaada wa hundi ya sh. milioni tano kutoka Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania, ambayo ilikadhiwa kwake na Mkurugenzi Mkuu Fadhili Manongi.
“Bado misaada inahitajika tunaendelea kutoa wito kwa watu walioguswa kuweza kutoa michango yao ili kuweza kusaidia shughuli za ujenzi na mahitaji ya wanafunzi walianza shule mfano madaftari, vitabu na huduma zingine zinazohusiana na elimu,”
alisema.
Aliongeza kuwa changamoto nyingine iliyopo ni kujenga nyumba za walimu na kliniki ya wakinamama na watoto,hivyo aliwaomba Watanzania, taasisi, mashirika na watu binafsi walioguswa kuendelea kuchangia.
Wakati huohuo, Chama cha Wafanyabiashara wa Kichina Tanzania (CBCT),kilikabidhi hundi kivuli yenye thamani sh. milioni 10 ya michango ya vitu mbalimbali kwa ajili ya wahanga hao kwa Mkuu huyo, ambayo ilikabidhiwa katika sherehe ya mwaka mpya wa Kichina kwa Makamu wa Rais Dk Mohammed Gharib Bilal juzi usiku.
Hundi hiyo ilikabidhiwa kwa Sadick na Mwenyekiti wa CBRT Zhu Jinfeng, ambapo alisema misaada mingine imendelea kutolewa hivyo michango hiyo hadi leo(jana) imefikia sh. milioni 12,550,000.
Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa mkoa alisema agizo la kuangalia uwezekano wa kuwapatia viwanja wapangaji liko palepale na watalitekeleza kama alivyoagiza Rais Jakaya Kikwete, hivyo utaratibu utaanza mara baada kukamilisha zoezi la wamiliki.
Aliongeza kuwa utaratibu huo wa wapangaji pia unahitaji fedha kwa ajili ya kufanya tathimni mpya utoaji wa fidia kwa wananchi watakaopisha maeneo hayo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment