Jan 12, 2012
WAFUGAJI NG'OMBE MKOANI NJOMBE WAOMBA KUPATIWA HUDUMA YA UHAMILISHAJI.
Wafugaji wa ng’ombe wa maziwa katika mkoa mpya wa Njombe wameiomba serikali kuwasaidia kupata huduma ya uhamilishaji ili waweze kupata mbegu bora ya ng’ombe wenye uwezo wa kutoa maziwa kwa wingi.
Akisoma risala ya kikundi cha ufugaji ng’ombe wa maziwa cha tupendane kwa mkuu wa mkoa wa Iringa Dk. Christine Ishengoma alipotembelea kikundi hicho kilichopo katika kijiji cha Magoda wilayani Njombe Bi. Christina Mutenzi amesema kuwa kutokana na kukosekana kwa huduma za uhamilishaji kiwango cha uzalishaji maziwa kimeshuka kutoka wastani wa lita 18 kwa siku mwaka 2000 hadi lita 12 kwasasa.
Akielezea sababu za kukosekana kwa huduma hiyo mtaalamu wa mifugo wa mkoa wa Iringa Bw. Paul Msangi amesema tatizo hilo linatokana na kwa baadhi ya vifaa kama maji ya kuhifadhia mbegu hizo yaani ’liquid nitrogen’ kwani huagizwa kutoka kituo kinachozizalisha huko mkoani Arusha hali inayofanya gharama za upatikanaji kuwa za juu na kuongeza kuwa katika kipindi cha mwaka huu wamepanga kuwatumia
baadhi ya wafugaji wakubwa ili kuweza kuwafikia wakulima wengi huku mkuu huyo wa mkoa akiagiza zoezi hilo lipewe umuhimu ili kuwatia moyo na kuwainua wafugaji wadogo.
Kikundi cha Tupendane kilianzishwa mwaka 2000 ambapo pamoja na ufugaji wa ng’ombe wa maziwa pia kinajishughulisha na kilimo cha mazao ya mboga na matunda kwa kutumia njia za asili kikiwa na wanachama 32 na jumla ya Ng’ombe wa maziwa 97.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment