HOME

Jan 17, 2012

NAKUAGAJE REGIA?

Mhe. Regia Mtema



















Siku zote ninaamini katika sera za vizazi kufundana na kukabidhiana majukumu. Katika maisha ya kijamii ninaumizwa sana na kupotea kwa utamaduni wa wazazi kurithisha watoto wao masuala kama ufundi na hata majukumu ya kitamaduni kwenye mila na desturi zetu. Ndio maana hivi sasa kwenye vijiji vingi hapa nchini imekuwa nadra kupata mafundi Seremala wa kurithi ama Waashi pia. Kwenye Siasa Kizazi kinaposhindwa kuandaa kizazi kingine kuchukua jukumu la kuongoza kuna hatari kubwa ya Taifa kukosa viongozi walioandaliwa vema na hivyo kuongoza inavyopasa. Taifa huumia sana linapopoteza viongozi wanaoandaliwa kubeba majukumu mazito ya kitaifa.


Dada Regia Estelatus Mtema, Mbunge wa Viti Maalumu, Waziri Kivuli wa Kazi na Ajira na Mjumbe wa Kamati Kuu CHADEMA ni mmoja wa wanasiasa vijana waliokuwa wanafundwa kuchukua majukumu zaidi ya Taifa letu. Alikuwa anafundwa na Chama chake. Alikuwa anafundwa na Bunge (mafundo kutoka kwa vyama vyote na hasa Spika Anna Simamba Makinda). Alikuwa anafundwa na marafiki zake. Alikuwa anafundwa na Chama cha Walemavu Tanzania (CHAWATA). Alifundwa na Shirika la FES. Dada Regia alikuwa anafundika. Alikuwa ni Hazina kubwa kwa Taifa letu. Alikuwa na sifa za peke yake kabisa kulinganisha na wanasiasa wengine na hasa wanasiasa vijana. Nitaeleza.


Sijui ni kwa nini mama yangu Bi Hajjat Shida Salum amekuwa sasa anapata habari kwanza kabla yangu (yeye ndiye aliyenipa habari za msiba wa Mwenyekiti wa Mkoa wa Shinyanga na Rafiki yangu kipenzi Shelembi).


Nikiwa nimepumzika sebuleni, nyumbani kwetu Tabata Bi Shida ghafla ananiuliza, umeongea na dada yako? Ilikuwa kama saa sita mchana hivi, yeye kasimama upenoni mwa ukuta ananiangalia macho makali. Nikashtuka kidogo maana amekuwa mgonjwa mgonjwa toka amerejea toka Hijja miezi kadhaa iliyopita. Najua akiniuliza hivyo ana maanisha nani (Mhonga Said Ibrahim Ruhwanya), nikamjibu sijazungumza naye, kunani? Akaniambia piga simu makao makuu nasikia kuna Mbunge wetu wa Viti Maalumu amepata ajali. Mara moja nikashika simu kumpigia ndugu Msafiri Mtemelwa. Alichoniambia sikuamini. Eti kwamba Regia amepata ajali na amefariki muda mfupi uliopita. Nikamwita rafiki yangu Hatibu Mchange anayeishi jirani yetu kumwambia aje ili anisindikize makao makuu ya chama. Kisha nikamjulisha Bi Shida kuhusu msiba wa rafiki yake na mwanae Regia. Nikamwacha akilia sana. Sikumpa pole wala kumtaka asilie maana kwanza sikuamini kabisa kwamba ni kweli Regia ametutoka. Nikasema mpaka nikamwone mwenyewe kwa macho yangu.


Siku nne kabla ya kifo chake Regia alikuja nyumbani kumsalimu mama yetu (Bi Shida siku zote alimwona Regia kama mwanaye na yeye Regia alimheshimu mama yangu kama mama yake mzazi kabisa). Wakati namsindikiza akaniambia, ‘ naona umeshikia bango suala la ajira kwa vijana. Nakuunga mkono na unipe ‘data’ za kutosha ili kupitia Wizara yangu nilisukume suala hilo kwa nguvu zaidi’. Tukakubaliana. Tukakumbatiana na kuagana. Yeye alikuwa ameambatana na kulwa wake Remija. Kumbe ndio nilikuwa namuaga moja kwa moja dada yangu Regia Estelatus Mtema, mwanasiasa kijana asiye na woga na jasiri haswa. Hii ndio sifa yake kubwa kuliko wanasiasa wengi vijana. Ujasiri!


Regia hakuwa mwanasiasa wa asili ama kurithi. Aliamua kuingia kwenye siasa kwa kwanza ushahiwishi wa ndugu David Kafulila ambaye walikutana huko kwenye Programu ya Mafunzo kwa vijana (YLTP) inayoendeshwa na Shirika la Friedrich Ebert Foundation (FES), mimi ni mwanzilishi wa Programu hii katika YLTP 1. David akiwa mwakilishi wa CHADEMA na Regia akiwa Mwakilishi wa CHAWATA katika YLTP 6. Regia alishawishika na kuingia CHADEMA, chama kikamweka kitengo cha Vijana kama Afisa. Wakati fulani kukatokea matatizo kati yake na Afisa mwenzake ndugu Ali Omar Chitanda kuhusu namna ya kufanya kazi. Regia akiwa na hoja kwamba chama kinajenga ushawishi kwa wasomi na hivyo vijana wasomi tu ndio waendeshe kitengo kile. Wakawa hawawezi kufanya kazi na mwenzake kabisa. Nikiwa Naibu Katibu Mkuu wa chama nikachukua maamuzi ya kumhamisha Regia na kumpeleka kuwa Afisa wa Mafunzo chini ya Kurugenzi ya Mafunzo na Oganaizesheni inayoongozwa na ndugu Benson Kigaila Masalamakali. Regia kwa ujasiri akaniandikia ujumbe mfupi wa simu ‘uamuzi wako sio sahihi’. Sikumjibu bali nikamwita Ofisini siku ya Pili yake. Nikamweleza namna ambavyo chama kinahitaji kada zote na kwamba wasomi wa vyuo vikuu waje kwenye chama wakijua pia kuna maafisa ambao si wasomi na wana mchango mkubwa katika harakati za kidemokrasia. Nikampa mifano ya namna mtu Kama Samora Machel alivyochaguliwa kiongozi wa FRELIMO ilhali kulikuwa na wasomi zaidi yake kama Joachim Chisano au hata mkewe Graca Machel. Regia alinielewa vizuri sana na mkutano ukaishia kutaniana kuhusu namna ya mitindo ya uongozi. Regia hakuficha kama hakupenda jambo na wala hakuwa anaangalia cheo cha mtu. Alisema anachokiamini na mengine yatabaki mjadala wa baadaye.


Ujasiri wake wakati mwingine ulimletea shida kwa wakubwa zake lakini hakuna hata mmoja aliyetilia shaka mapenzi yake kwa chama chetu. Hakujali kuudhiwa na alikuwa tayari kukilinda chama muda wote. Huu ni mfano wa pili wa Ujasiri wake kisiasa.


Wakati wa uchaguzi Mkuu wa nchi mwaka 2010 Regia alikwenda kugombea Ubunge katika Wilaya ya nyumbani kwao Kilombero. Watu wengi hawakumpa nafasi kubwa ya kushinda. Aliliandaa jimbo lake kwa mikutano ya mara kwa mara. Alishinda kura za maoni katika mchakato wa ndani ya chama. Katika kikao cha Kamati Kuu mmoja wa Wakurugenzi wa Chama akasema tunaye mgombea mwingine mzuri sana, Mwanasheria. Regia akaombwa kukaa pembeni. Akakubali. Kamati Kuu ikampitisha mtu ambaye hakwenda kwenye kura za maoni na wala hatukuwa tunamjua maana tuliambiwa na mtu tunayemwamini kwamba ni mgombea mzuri. Regia hakufurahishwa na uamuzi ule lakini kwa heshima na utiifu wa hali ya juu akakubali kutogombea. Siku za kurejesha fomu za kugombea zilipokuwa zinakwisha yule mgombea akatoa nje. Hakuonekana, kwa sababu mbalimbali ambazo sisi tuliokuwa mbali na Dar es Salaam na Morogoro hatuzijui. Chama hakikuwa na namna isipokuwa kurudi kwa Regia kumwomba aokoe jahazi. Regia hakusita. Akaendesha kampeni za uhakika akiwa hana mali wala jina kisiasa. Akaaminiwa na watu wa Kilombero. Akapata kura nyingi sana ambazo hata zilileta utata wa uhalali wa matokeo ya uchaguzi katika Jimbo lile. Ujasiri na nidhamu ya namna hii ni nadra sana kwa wanasiasa sio tu vijana hata waliobobea kwenye siasa. Huyu ndio Regia. Ndiye tunamsindikiza kwenye nyumba yake ya milele. Regia mwenye upendo wa dhati kwa watu aliowapenda. Regia aliyekuwa tayari kusaidia kwa hali na mali wenzake wanapohitaji msaada. Hii ni sifa yake ya nyingine ya kipekee.


Mara baada ya Uchaguzi Mkuu na yeye kuchaguliwa kuwa Mbunge wa Viti Maalumu, Spika alitugawa kwenye Kamati Wabunge wote. Kazi ya kwanza ya Kamati hizi ilikuwa ni kuchagua wenyeviti na makamu wao. Regia alijua mimi napenda kuendelea kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Mashirika ya Umma (uwekezaji umma). Hata hivyo alijua nina wakati mgumu sana kutokana na mazingira ya kisiasa yaliyokuwapo wakati ule kati ya Wabunge wa CCM na CHADEMA. Regia ni Mbunge pekee (ukiachana na wajumbe wa kamati ya POAC kutoka CHADEMA) aliyezunguka nami usiku kucha na kupiga simu kwa kila Mbunge mjumbe wa Kamati yangu kuniombea kura. Mbunge mwenzangu na Rafiki yangu wa karibu kutoka Ludewa Deo Filikunjombe atamkumbuka Regia kwa aina ya kampeni aliyopiga. Deo aliniambia kwamba alipokea simu ya mwanamke anaongea Kipangwa (moja ya Lugha ya watu wa Ludewa). Mwanamke yule mwenye sauti nyembamba na ya kutulia alikuwa anamwombea kura Zitto kuwa mwneyekiti wa POAC. Deo alifurahishwa na namna Regia alivyoweza kutumia lugha ya nyumbani kwao kuniombea kura. Hata tulipopata taarifa kwamba Kamati ya Wabunge wa CCM imeamua kwamba atakayepewa kura sio mimi, Regia alinitia moyo na kuendelea na kampeni. Asubuhi ya siku ya kura alimpitia kila mjumbe wa Kamati POAC aliyemwona na kumkumbusha kunipa kura hata kama CCM imewakataza. Nilimcheka sana Regia kwa kumwambia wewe sio mzoefu hapa. Hao wakishakaa ndio maamuzi hayo. Akaniambia hapana watabadilika. Ghafla Waziri Mkuu akatangaza kikao kingine cha Wabunge wa CCM na huko wakaelezwa kwamba kamchagueni Zitto. Ningekata tamaa bila kuendelea na juhudi usiku kucha kama nilivyoshauriwa na regia kwa kweli nisingeshinda nafasi ile. Regia alikuwa mtu wa kwanza kumjulisha matokeo ya uchaguzi nilipopata kura 13 kati ya 15 zilizopigwa. Huyu ndiye Regia ambaye alikuwa na uwezo wa kufanya kila mbinu ili mwenzake apate msaada. Ni lazima watu watoe machozi. Ni lazima Wabunge watoe machozi. Ni lazima wana CHADEMA wamlilie. Mimi sitawafuta machozi na nimekataa kulia.


Kikao cha mwisho cha chama ambacho nilishiriki na Regia nilihudhuria kwa muda mfupi sana. Wenzangu watakumbuka mengine katika kila kikao kile. Mimi ninakumbuka moja tu ambalo ni moja ya sifa pekee aliyokuwa nayo na wanayo wanasiasa wachache sana na hasa wanasiasa vijana (ambao hupenda zaidi siasa za kuridhisha kwa kusema watu wapendacho). Regia alikuwa na uwezo mkubwa wa kusema usichopenda kusikia. Alisema tu. Katika kikao kile wajumbe na Wabunge walikuwa katika ‘emotion’ sana kuhusiana na muswada wa mchakato wa kuandika Katiba. Mjadala ulikuwa mkali sana. Mwenyekiti wetu akampa nafasi Regia aseme. ‘mimi nashauri tuombe kuonana na Rais Kikwete’ yalikuwa ni maneno yake makali kupenya kwenye ngome za masikio ya wengi na yalipokelewa kwa mguno mkubwa. Mwenyekiti akaamrisha wajumbe na Wabunge watulie kwani Regia ana haki ya kutoa maoni yake. Mimi niliondoka baada ya muda mfupi maana nilikuwa ndio nimetoka nchini India kwa matibabu na nilikuwa na masharti ya kupumzika muda mrefu. Ushauri wa Regia (pamoja na wajumbe na viongozi wengine wa chama walioshauri ama waziwazi au kwa chinichini) ndio uliofuatwa na sasa kumekuwa na mazungumzo ya mara kwa mara ya viongozi kuhusu sheria ile ya mchakato wa kuandika Katiba. Huyu ndio dada Regia. Maisha mafupi lakini mafunzo makubwa katuachia vijana wenzake kwenye medani ya siasa.


Nakuagaje Regia?


Nilikataa kuamini kuwa umekufa. Nikasema mpaka nikuone.


Nilipofika Tumbi, nikasema hujafa na wala siingii ‘motury’ kukuona.


Sasa eti nakuandikia Tanzia . Kwa nini nikuage?


Halafu nakuagaje REGIA?


Ukikutana na Shelembi Magadula, mwambie kile kiti chake cha udiwani tulikitunza, akija atakikuta. Ukikutana na Chacha Wangwe Mwambie bado tunaendelea na harakati Nyamongo. Ukikutana na Amina mwambie asilie tena vijana wengi wameingia Bungeni na sasa wanaelekea Ikulu.


Ukikutana na Bibi Titi mwambie sasa wanawake hata wanawake walemavu wanaweza bila hata kuwezeshwa, wanajiwezesha.


Nakuagaje dada yangu mpenzi? Haya.


Mungu atupe subira.


Kabwe Zuberi Zitto, Mb


DSM, 16 Januari 2012.

No comments:

Post a Comment