HOME

Jan 12, 2012

EWURA KUTANGAZA BEI MPYA ZA UMEME LEO!!

Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura), leo inatarajia kutangaza bei mpya ya umeme.


Taarifa ya Ewura iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari imesema kuwa hatua hiyo imefikiwa baada ya mamlaka hiyo kukamilisha mchakato wa kupitia maombi ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) na maoni ya wadau waliopinga.


“Kesho Ewura itatangaza bei mpya za huduma za umeme kama Tanesco ilivyowasilisha maombi mwishoni mwaka jana,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo iliyosainiwa na Meneja Uhusiano, Titus Kaguo.Wiki iliyopita, Kaguo alisema wamekamilisha maombi ya Bodi ya Wakurugenzi ya Ewura iliyowataka kupitia upya maombi ya Tanesco kutaka kupandisha bei hiyo.


Amesema Ewura ilikwishakamilisha taratibu zote na kilichokuwa kinasubiriwa ni kutangaza bei mpya. Hata hivyo, akiwafariji wananchi akiwataka wasiwe na wasiwasi kwani wamezingatia kiwango cha mapato.


“Tuko makini kuhakikisha usawa wa huduma hii muhimu kwa jamii haiathiri pande hizi mbili ambazo kimsingi zinategemeana, nawaomba wananchi wawe wavumilivu wakati tukikamilisha kazi ya uchunguzi,” alisema.


Hatua hiyo inafanyika baada ya Tenesco kuwasilisha Ewura mapendekezo ya kupandisha gharama za umeme kwa bei ya wastani ya kuuza umeme iliyopo sasa ya Sh141 kwa uniti hadi Sh359 kwa uniti kuanzia Januari mwaka huu, ongezeko hilo ni sawa na asilimia 155 ya bei ya sasa.


Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, William Mhando amesema sababu ya kupandisha bei ya umeme ni kiliwezesha shirika hilo kukabiliana na ongezeko la gharama za uendeshaji zinazotokana na juhudi za kuondoa mgawo wa umeme.


Mhando amesema athari ambazo zitapatikana ikiwa bei haitaongezwa ni shirika kushindwa kufanya uwekezaji na kutekeleza miradi mbalimbali ikijumuisha uuganishaji wateja wapya.

No comments:

Post a Comment