HOME

Jan 27, 2012

MAZUNGUMZO YA RAIS JAKAYA M. KIKWETE NA WAZIRI MKUU WA UINGEREZA!!


Tanzania imepongezwa kwa kuwa mfano bora na wa kuigwa katika kuleta mabadiliko chanya kwenye Sekta za Kilimo na Elimu barani Afrika.

Waziri Mkuu wa Uingereza Bw. David Cameron ametoa  pongezi hizo kwa Rais Kikwete wakati wa mazungumzo yao jana jioni hapa Davos ambapo wote wawili wanahudhuria mkutano wa Kiuchumi Duniani wa kila mwaka, maarufu kama World Economic Forum (WEF), ambapo masuala  ya uchumi, athari mbalimbali zinazokabili uchumi duniani kwa sasa na jitihada mbalimbali zinazofanywa kunusuru uchumi huo na njia  za kuleta mabadiliko chanya ya kukuza uchumi barani Afrika yanajadiliwa.

“Afrika inapitia kipindi cha mabadiliko ambayo ni chanya, na Tanzania ni mfano bora wa kuigwa katika hili”. Bw. Cameron amemueleza Rais Kikwete.

Katika mazungumzo yao Rais Kikwete amemueleza Bw. Cameron kuwa kilimo ni sekta kubwa na inayotegemewa na Watanzania wengi na kwamba serikali inalenga  katika kukuza kilimo kwa ajili ya kujitosheleza kwa chakula ndani na nje ya nchi.

Rais Kikwete na Bw. Cameron pia wamezungumzia masuala mbalimbali yanayohusu siasa na usalama barani Afrika.

Mapema jana asubuhi, Rais Kikwete amejumuika na viongozi wengine kutoka Ethiopia, Guinea-Conackry, Kenya na Afrika Kusini  kuzungumzia mabadiliko mbalimbali ya uchumi na maendeleo  barani Afrika.

Katika mjadala huo uliongozwa na Waziri Mkuu wa Zamani wa Uingereza Bw. Gordon Brown, Rais Kikwete amesema pamoja na mabadiliko hayo, bara la Afrika nalo ni sehemu ya Dunia Uchumi, hivyo nayo kupata athari mbalimbali zinazotokana na  mabadiliko hayo ya Kiuchumi duniani.

Rais amesema pamoja na athari na mabadiliko ya Kiuchumi duniani, bado Afrika ina mahitaji zaidi katika kutekeleza sera zinazolenga katika uchumi imara na kuwekeza zaidi katika sekta za elimu, utafiti, kilimo, viwanda na miundombinu.

Rais Kikwete pia amefanya mazungumzo na viongozi na wadau mbalimbali wa maendeleo wakiwemo Bw. Bill Gates, pamoja na viongozi wa Ethiopia na Kenya ambapo wamezungumzia namna ambayo Bw. Gates atatoa mchango wake zaidi katika masuala ya kilimo na utafiti.

Rais Kikwete amekutana na kufanya mazungumzo na Mama Sadako Ogata Rais wa Shirika la Misaada la Japan, maarufu kama Japan  International Cooperation Agency (JICA)  ambaye naye ameelezea kuwa JICA itaendelea kutoa misaada mbalimbali kwa Tanzania pamoja na kwamba yeye amefikia kipindi chakustaafu.

Rais Kikwete pia amekutana na kufanya mazungumzo na  Mkurugenzi Mtendaji wa Vodafone, Bw. Vittorio Colao ambaye ameonesha nia ya kusaidia Tanzania katika kutoa na kusambaza elimu  kwa kutumia simu za mkononi katika masuala mbalimbali ya afya, kilimo na elimu.

Mwisho.

Imetolewa na Premiere Kibanga,
Mwandishi wa Habari Msaidizi wa Rais,
Davos-Switzerland.
27 Januari, 2012

No comments:

Post a Comment