HOME

Feb 6, 2012

CHINA YACHANGIA MAFURIKO,AJALI YA MELI YA MELI ZANZIBAR!!

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akizungumza na Balozi wa China nchini Tanzania, Liu Xinsheng, aliyefika ofisini kwake Ikulu Dar es Salaam leo Februari 6, 2012 kwa ajili ya kumuaga baada ya kumaliza muda wake nchini.



Ubalozi wa China kwa kushirikiana na Jumuiya za wananchi wa China wanaoishi  nchini Tanzania wametoa jumla ya Dola za Kimarekani 10,000 kwa ajili ya kusaidia maafa ya mafuriko na ajali ya meli huko Zanzibar.


Kati ya fedha hizo Dola za Kimarekani 5,000 zimetolewa kwa ajili ya kusaidia wahanga wa mafuriko mkoani Dar es salaam na Dola za Kimarekani 5,000 zilizobaki kwa ajili ya kutoa pole kwa familia zilizopoteza ndugu zao katika ajali ya meli ya MV Spice Islanders iliyozama kwenye mkondo wa Nungwi huko Zanzibar.


Akikabidhi hundi hizo kwa Makamu wa Rais Dk. Mohammed Gharib Bilal ofisini kwake Ikulu alipofika kwa ajili ya kumuaga Balozi wa China nchini anayemaliza muda wake Liu Xinsheng  alisema msaada huo  ni kutimiza ahadi waliyoitoa wakati wa
kusherehekea mwaka mpya wa Kichina ambapo Makamu wa Rais alikuwa mgeni rasmi.

Liu aliishukuru serikali ya Tanzania na wananchi kwa ujumla kwa ushirikiano waliompa kiasi cha kumwezesha kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi katika kipindi chote alichokaa nchini cha karibu miaka minne.


“Nimekuja kukuaga baada ya kukaa nchini karibu miaka minne na nusu. Naichukulia Tanzania kama nyumbani. Nawaona Watanzania ni marafiki na ndugu wa karibu.

Ushirikiano mlionipa umeniwezesha kutekeleza majukumu yangu vizuri,” alisema Liu.

Alisema katika kipindi hicho amefanikisha kujengwa kwa uwanja wa Taifa, ukumbi wa mikutano, hospitali ya moyo ambayo ametia saini leo kwa ajili ya kuanza ujenzi  na kusema misaada kutoka imeongezeka toka Dola za Kimarekani  700,000 milioni mwaka
2007 hadi Dola za Kimarekani 2.1 bilioni mwaka jana.


Katika mazungumzo hayo Makamu wa Rais amemshukuru Balozi huyo kwa msaada huo kwa wahanga wa mafuriko pamoja na wa ajali ya meli Zanzibar na kumhakikishia kwamba uhusiano kati ya nchi hizo mbili utaendelea kuimarishwa.


Dk. Bilal alitumia fursa hiyo pia kuishukuru Serikali ya China kwa misaada yake mbalimbali kwa Tanzania akitolea mfano wa mradi wa Liganga na Mchuchuma ambao unatekelezwa kwa pamoja na Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) na Kampuni za Kichina
ambao anaamini utakuwa wa mafanikio.

No comments:

Post a Comment