Feb 9, 2012
WILAYA YA KISHAPU YATISHA KWA UBADHIRIFU WA FEDHA ZA UMMA!!
Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) imebaini ubadhirifu mkubwa wa fedha za serikali kiasi cha shilingi bilioni 7 kufuatia ukaguzi maalum uliofanyika katika Halmashauri ya wilaya ya Kishapu, mkoani Shinyanga.
Akizungumza na waandishi wa habari leo mjini Dodoma wakati wa kuwasilisha ripoti za matokeo ya kaguzi 5 za ufanisi/Thamani ya fedha Mdhibiti na Mkaguzi mkuu wa Hesabu za Serikali Bw. Rudovick Utouh akiwa ameambatana na baadhi ya wenyeviti wa kamati za kudumu za Bunge amesema kuwa Ofisi yake imebaini matukio 14 yenye jumla shilingi bilioni 7 ambayo yana kila dalili za ubadhirifu wa fedha za umma.
Bw. Utouh amefafanua kuwa ofisi yake imebaini ubadhirifu huo kufuatia uhakiki wa kina na ukusanyaji wa ushahidi kuhusiana na hati za malipo zilizokosekana wakati wa ukaguzi uliopita wa mwaka wa fedha 2009/2010 na pia kufanya mahojiano na viongozi na wahasibu ambao wanahusika na utunzaji wa nyaraka za malipo ili kubaini ukweli kuhusiana na upotevu wa hati hizo za malipo.
Amesema wataalam wa ofisi yake katika kubaini ubadhirifu huo ilipitia hati zote za malipo sanjari na kuhakiki stakabadhi za malipo ili kujua uhalali wa malipo yaliyofanywa na Halmashauri bila kuidhinishwa na mkurugenzi wa Halmashauri pamoja na kufanya mahojiano na viongozi mbalimbali wa Halmashauri hiyo ili kupata maoni yao.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment