HOME

Apr 16, 2012

RAIS KIKWETE AWASILI BRAZIL KWA ZIARA YA KIKAZI YA SIKU TANO!!

Mke wa Rais Mama Salma kikwete akipokea shada la maua mara baada ya
yeye na Rais Jakaya Mrisho Kikwete kuwasili Jumapili Aprili 15, 2012 katika
hoteli ya Tivoli jijini Sao Paulo, Brazil, tayari kwa ziara ya siku tano ya
kikazi nchini humo. Kulia kwake ni Rais Kikwete na nyuma kulia ni  Waziri
wa kazi na Uwezeshaji Wanachi Kiuchumi na Ushirika wa Zanzibar Mh Haroun
Ali Suleiman na mwenye miwani ni Balozi wa Tanzania nchini Brazil, Mh
Francis Malambugi.
Rais Jakaya Mrisho kikwete akiongea na Msaidizi Mwandamizi wa Rais
(Diplomasia) Balozi Liberata Mulamula baada ya mkutano wa maandalizi ya
ziara yake ya siku tano nchini Brazil Jumapili Aprili 15, 2012 katika
hoteli ya Tivoli jijini Sao Paulo. katikati  ni  Waziri wa kazi na
Uwezeshaji Wanachi Kiuchumi na Ushirika wa Zanzibar Mh Haroun Ali Suleiman.
Rais Jakaya Mrisho kikwete na Mama Salma Kikwete  wakiwasili Jumapili
Aprili 15, 2012 katika hoteli ya Tivoli jijini Sao Paulo, Brazil, tayari
kwa ziara ya siku tano ya kikazi nchini humo. Kulia ni  Waziri wa kazi na
Uwezeshaji Wanachi Kiuchumi na Ushirika wa Zanzibar Mh Haroun Ali Suleiman.
Rais Jakaya Mrisho Kikwete akipeana mikono mwandishi mwandamizi wa
Habari Leo na Daily News, Bw Joseph Lugendo, alipokuwa analakiwa baada ya
kuwasilii   Jumapili Aprili 15, 2012 katika hoteli ya Tivoli jijini Sao
Paulo, Brazil, tayari kwa ziara ya siku tano ya kikazi nchini humo
Rais Jakaya Mrisho Kikwete akipeana mikono na kaimu Mkurugenzi Mtendaji
wa Kituo cha Uwekezaji (TIC) Bw Raymond Mbilinyi,   baada ya kuwasili
Jumapili Aprili 15, 2012 katika hoteli ya Tivoli jijini Sao Paulo, Brazil,
tayari kwa ziara ya siku tano ya kikazi nchini humo
Rais Jakaya Mrisho kikwete amewasili  Brazil kwa ajili ya ziara ya kikazi ya siku tano.


Katika ziara hiyo Rais Kikwete anatarajia kukutana na kufanya mazungumzo na mwenyeji wake Rais Dilma Varna Rousseff wa Brazil  na Rais mstaafu wa nchi hiyo Mh. Inacio da Silva Lula na viongozi waandamizi wa nchi hiyo.


Katika ziara hiyo, Rais Kikwete atahudhuria mkutano wa mwaka wa wakuu wa nchi zinazoshiriki katika Mpango wa Ubia wa Uwazi Serikalini (Open Government Partnership-OGP) utakaofanyika mjini Brasilia chini ya Uenyekiti wa Rais Rousseff na kuhudhuriwa na wajumbe wapatao mia nne (400) kutoka serikalini, Asasi zisizo za kiserikali, Sekta binafsi pamoja na Mashirika ya Kimataifa.

 Ubia wa Uwazi Serikalini au kwa kifupi OGP,  ni mpango uliozinduliwa  Septemba 2011 mjini New York,  Marekani kwa lengo la kuwapa wananchi nafasi ya kushiriki  katika kuamua mambo yanayowahusu, kupitia vyama visivyo vya Kiserikali na vya Kijamii.

Ubia huu unashirikisha kwa usawa wawakilishi wa serikali kwa upande mmoja na wawakilishi wa Asasi zisizo za Kiserikali za Kijamii kwa upande mwingine. Nchi ya Brazil kwa kushirikiana na Marekani imekuwa mstari wa mbele katika kusukuma ubia huu.

Rais Kikwete anatarajiwa kuhutubia mkutano huo tarehe 17 Aprili, asubuhi mara tu baada ya hotuba ya  ufunguzi itakayotolewa na Mwenyekiti wa mkutano huo Rais Dilma Rousseff wa Brazil, ambapo ataelezea maendeleo iliyofikia katika kuandaa mpango kazi wa kutekeleza ahadi ya kuongeza uwazi kama ilivyokubaliwa katika kikao kilichofanyika Disemba 2011.

Rais Kikwete anatarajiwa kurejea nchini tarehe 20 Aprili, 2012.

No comments:

Post a Comment