Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Jaji Joseph Warioba akiongea na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Kulia ni Katibu wa Tume, Bw. Assaa Rashid. (Picha na Tume ya Katiba) |
Tume ya Mabadiliko ya Katiba imesema imejipanga kuandaa rasimu ya katiba itakayoweka mbele maslahi ya taifa na kuwaomba wananchi waijadili na kutoa maoni yao katika mabaraza ya katiba yatakayokutana kuanzia mwezi Juni mwaka huu.
Mwenyekiti wa Tume hiyo Jaji Jospeh Warioba amesema leo jijini Dar es Salaam kuwa katika kuandaa rasimu hiyo, Tume yake haitapokea shinikizo kutoka taasisi, asasi, makundi au vyama vya siasa.
“Tume haitengenezi katiba ya vikundi au vyama, tunaandaa katiba ya nchi,” amesema Jaji Warioba katika mkutano wake na waandishi wa habari katika ofisi za Tume na kufafanua kuwa Tume inazingatia uzito wa hoja zilizotolewa na wananchi na sio idadi ya watu waliotoa maoni.
Jaji Warioba amewataka wananchi kutokubali kutumiwa na makundi, asasi, taasisi na vyama wakati wa kujadili na kutoa maoni katika mabaraza ya katiba ya wilaya.
Akizungumza kuhusu ushiriki wa walemavu katika mabaraza ya katiba, Jaji Warioba amesema Tume yake inatarajia kuunda mabaraza ya Katiba ya watu wenye ulemavu ili kuwapa fursa walemavu kutoka Tanzania Bara na Zanzibar kutoa maoni yao kuhusu rasimu ya Katiba itakayotolewa na Tume.
Hatua hii inafuatia ombi la Shirikisho la Vyama vya Watu wenye ulemavu Tanzania (SHIVYAWATA) na Umoja wa Watu wenye ulemavu Zanzibar (UWAZA) waliloliwasilisha kwa Tume.
Aidha, Jaji Warioba amezungumzia mafanikio na changamoto zilizojitokeza katika chaguzi zilizofanyika nchini kote hivi karibuni za kuchagua Wajumbe wa Mabaraza ya Katiba kuanzia ngazi ya mitaa, vijiji, vitongoji na shehia.
Kwa mujibu wa Jaji Warioba, tathmini ya Tume inaonyesha kuwa kwa kiwango kikubwa viongozi na watendaji katika ngazi za vijiji, mitaa, shehia na kata walizingatia mwongozo uliotolewa na Tume na kuwa maeneo mengi wananchi walichaguana kwa amani na utulivu.
“Kwa mfano jumla ya shehia 323 sawa na asilimia 96.4 kati ya shehia 335 kwa upande wa Zanzibar zimekamilisha vizuri mchakato huu, hali kadhalika jumla ya Kata 3,331 sawa na asilimia 99.8 kati ya Kata 3,339 kwa Tanzania Bara nazo zimekamilisha mchakato wa kuwapata wajumbe wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya kwa kuzingatia utaratibu uliotolewa kwa mujibu wa Mwongozo,” amesema Jaji Warioba.
No comments:
Post a Comment