HOME

Mar 1, 2012

SERIKALI YATOA MAGARI YA HUDUMA YA AFYA YA MKOBA!!


Na.Magreth Kinabo – Maelezo


Serikali kupitia Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii imetoa magari  saba  ya huduma  za mkoba  kwa ajili ya  kuwawezesha wananchi wengi kupata huduma za madaktari bingwa hususan walioko vijijini.


Kauli  hiyo ilitolewa  leo (jana) na Waziri wa Afya na  Ustawi wa Jamii, Dk. Hadji Mponda  wakati akizungumza na waandishi wa habari kabla ya kukabidhi magari hayo kwa wawakilishi wa hospitali mbalimbali kwenye ukumbi wa mikutano wa wizara hiyo.


“Tunagawa magari haya kwa madhumuni ya kupeleka huduma za wataalamu bingwa karibu na wananchi.


 “Lengo la Serikali ya Awamu ya Nne ni kuhakikisha huduma za afya na ustawi wa jamii zinawafikia nchinii kote na hasa vijijini, ambako ndipo wanapoishi wananchi wengi. Haya magari yatatumiwa na madaktari bingwa katika kanda zetu zote nchini kote,” alisema Waziri Mponda.


  Aliitaja thamani ya magari hayo kuwa ni sh. milioni 181 kwa kila mmoja ambayo inahusisha pamoja na vifaa vilivyoko ndani ya gari.


Waziri Mponda aliongeza kuwa watumishi kutoka hospitali husika watafundishwa namna ya kutumia magari hayo ambayo yana vifaa maalaum vipya vya kisasa, ambao watawaelekeza wenzao wakati wa kliniki hiyo.


 Alivitaja vifaa hivyo kuwa ni vya kufanyia uchunguzi na vya kutolea huduma. Magari hayo pia yana jenereta kwa ajili ya kupata umeme sehemu ambazo hazitakuwa na umeme.


 Hospitali zilizopata magari hayo  za Kanda ya Mashariki ni CCBRT  Dares Salaam, Kasikazini  KCMC  Kilimanjaro, Kati  Chuo Kikuu cha Dodoma Kusini  Rufaa ya Mbeya, Kusini Mashariki Ndanda Mtwara, Magharibi Maweni Kigoma na Ziwa Bugando.


Wakizungumzia kuhusu magari hayo wawakilishi wa hospitali hizo walisema wanaishukuru  serikali kwa kuwa utawezesha wananchi wasioweza kufikia huduma za afya kuzipata kwa kiurahisi.

No comments:

Post a Comment