Meneja wa Bia ya Kilimanjaro George Kavishe akizungumza jijini Dar es salaam leo. |
Tamasha la washindi wa tunzo za muziki Tanzania, zijulikanazo kwa jina la Kilimanjaro Tanzania Music Awards Winner’s Tour kwa mwaka huu zinafikia ukingoni Jumamosi hii ya tarehe 02 Juni, katika viwanja vya Posta, Kijitonyama jijini Dar es Salaam.
Huu utakuwa ni mkoa wa sita kufanyika tamasha hili kubwa na zuri ambalo lina dhana kuu tatu ambazo ni kwanza kutoa burudani kwa wapenzi wa bia ya Kilimanjaro Premium Lager ambao ndio wadhanimini wakuu wa mchakato mzima, Dhana ya pili ni kuwapa wasanii walioshinda tunzo nafasi ya kuonana na mashabiki wao na kuwashukuru kwa kushiriki vilivyo zoezi la upigaji kura na kuwawezesha kuwa washindi wa tunzo hizi kubwa na za kipekee katika ukanda wa Afrika ya Mashariki na Kusini mwa jangwa la Sahara. Na dhana ya tatu, ni kuwathibitishia mashabiki wao hao hao kwamba hawakubahatisha kupewa tunzo hizi, kwa kufanya onesho zuri litakaloacha msisimko wa mwaka mzima kutokana na ukubwa wake, na pia kwa kuzingatia kwamba wasanii wanaoshiriki tamasha hili ni wale ambao ni bora kabisa kwa kipindi hiki na ndio sababu wakatunukiwa tunzo.
Kabla ya Tamasha hili kubwa la Dar es Salaam, wasanii hawa wamepita takriban mikoa mitano huku shughuli za Tamasha zikiambatana na zoezi la kutafuta vipaji ambalo limefanikiwa kuibua vipaji sita ambavyo vitaonekana siku ya tamasha.
Mikoa ambayo Tamasha limepita ni mikoa ya Dodoma, Mwanza, Moshi, Mbeya na Mtwara ambapo kila mkoa ulitoa mshiriki mmoja chipukizi katika zoezi jipya la kutafuta vipaji lililopewa jina la Kilimanjaro Awards Talents Search, isipokuwa Dodoma tu iliyotoa washiriki wawili ambao walilingana alama.
Zoezi hilo lenye lengo la kuibua vipaji vya mikoani lilisimamiwa na Majaji wanne ambao ni Mshindi wa tunzo ya wimbo bora wa Reggae Queen Darleen, wanamuziki wakongwe wa muziki wa Bongoflava Profesa Jay na Juma Nature pamoja na Henry Mdimu, ambaye ni Mhariri wa Burudani wa kampuni ya Mwananchi Communications Limited.
Kutoka Dodoma, chipukizi waliopatikana, ambao watashiriki kwenye tamasha hili kubwa na la aina yake ni Issa Dubat na Juma Madaraka, kutoka Mbeya ni neema, kutoka Mwanza ni Christina, kutoka Moshi ni Sungura na kutoka Mtwara ni Nicolaus. Hawa ndio chipukizi kutoka mkoani ambao watafungua tamasha hili na kufuatiwa na washindi wa tunzo za Kili Mwaka huu ambao kwa idadi, watakuwa 14 kwa jumla.
Wasanii hao ni Diamond ambaye anashikilia tunzo tatu, Ommy Dimpoz ambaye ni msanii bora anayechipukia ambaye pia anashikilia tunzo ya wimbo bora wa AfroPop, Ally Kiba ambaye ni mtumbuizaji bora wa kiume, na Barnabas Elias ambaye ni msanii bora wa kiume kwa mujibu wa tunzo za Kilimanjaro za mwaka huu.
Wengine watakaopanda jukwaani ni pamoja na Roma Mkatoliki ambaye anashikilia tunzo ya mwanamuziki Bora wa Hip Hop ambaye pia amenyakua tunzo ya wimbo bora wa Hip Hop, Isha mashauzi ambaye amenyakua tunzo ya wimbo bora wa taarab, Suma Lee ambaye anashikilia tunzo ya wimbo bora wa mwaka, Queen Darleen, Kitokololo ambaye anashikilia tunzo ya rapa bora wa bendi, na AT ambaye ana tunzo ya wimbo bora wenye asili ya kitanzania.
Warriors from the East pia watapanda jukwaani wakiwa ni washindi wa wimbo bora wa reggae, The African Stars wana wa kutwanga na kupepeta pia watapanda na tunzo yao ya wimbo bora kabisa uliowahi kutokea msimu huu wa Dansi, Ben Pol atapanda kama mwanamuziki bora wa R&B na Bi Khadija Kopa atawakilisha kama mtumbuizaji bora wa kike.Tamasha litaanza saa kumi jioni ambapo kila mtanzania mpenda burudani atatozwa kiingilio cha shilingi za kitanzania 4000 na pia atapatiwa bia moja bure mlangoni.
Kilimanjaro Premium Lager inachukua fursa hii kuwakaribisha wadau wote wa burudani katika tamasha hili kubwa zuri, kuburudika na kutathmini kwa pamoja muelekeo wa sanaa yetu ya muziki.
No comments:
Post a Comment