HOME

May 6, 2013

TANZANIA YALAANI WALIOLIPUA BOMU ARUSHA!!

Serikali ya Tanzania imetoa tamko na kulaani waliohusika na mlipuko wa bomu jijini Arusha uliotokea wakati wa uzinduzi wa kanisa Katoliki parokia mpya ya Mtakatifu Joseph Mfanyakazi, eneo la Olasit jijini Arusha.

Waziri wa mambo ya ndani Dk. Emmanuel Nchimbi
Waziri wa mambo ya ndani Dk. Emmanuel Nchimbi ameliambia bunge mjini Dodoma leo kuwa mpaka sasa polisi inawashikilia watu 6 wakiwemo raia wanne wa kigeni na mmoja anayedaiwa kuwa alirusha bomu hilo ambaye ni dereva wa Bodaboda mwenye umri wa miaka 20 aliyefahamika kwa jina la Victor Ambrose kwa tuhuma za kuhusika na tukio hilo lililosababisha vifo vya watu wawili na wengine zaidi ya 50 kujeruhiwa kati yao watatu wakiwa katika hali mbaya.

Dk. Nchimbi amefafanua katika siku za hivi karibuni kumekuwa na jitihada za watu wachache wanaojaribu kuvunja amani ya nchi kwa kusababisha mapigano au vurugu serikali kwa nguvu zake zote haitasita kuwachukulia hatua kali wale wote wanaojihusisha na vitendo hivyo bila kujali hadhi au jina la mtu.

Amesema serikali inaungana na watanzania wote kulaani tukio hilo na kuahidi kuwatia mikononi wote waliohusika na mlipuko huo.

Aidha Dk. Nchimbi amesema uchunguzi wa awali umebaini kuwa kitu kilichosababisha mlipuko ni bomu ingawa bado uchunguzi unaendelea kujua ni la aina gani.

Wakati huo huo, rais Jakaya Mrisho Kikwete amelazimika kusitisha ziara yake ya kikazi nchini Kuwait na kurudi nchini kufanya tathmini na hatua za kuchukua kuhusu tukio hilo.

No comments:

Post a Comment