HOME

Jan 27, 2012

UNHCR YAFANYA MAZUNGUMZO NA TANZANIA KUWAREJESHA WATANZANIA WAISHIO SOMALIA!!

Mwakilishi wa Shirika hilo nchini Tanzania Bw. Oluseyi Bajulaiye


















Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuwahudumia Wakimbizi (UNHCR) linafanya mazungumzo na serikali ya Tanzania katika kufanikisha kuwarejesha nyumbani raia 200 wa Tanzania wanaoishi nchini Somalia.


Mwakilishi wa Shirika hilo nchini Tanzania Bw. Oluseyi Bajulaiye amesema serikali inataka kwanza kujiridhisha kwa kuwahakiki watanzania hao waliopo mjini Mogadishu, kabla ya kuridhia warejee nchini.


Bw. Bajulaiye amesema UNHCR inatarajia kuwarejesha nchini mwezi ujao raia hao wa Tanzania ambao wengi wao wanatokea visiwani  Zanzibar na waliondoka nchini mnamo miaka ya 2001 na 2005.

MAZUNGUMZO YA RAIS JAKAYA M. KIKWETE NA WAZIRI MKUU WA UINGEREZA!!


Tanzania imepongezwa kwa kuwa mfano bora na wa kuigwa katika kuleta mabadiliko chanya kwenye Sekta za Kilimo na Elimu barani Afrika.

Waziri Mkuu wa Uingereza Bw. David Cameron ametoa  pongezi hizo kwa Rais Kikwete wakati wa mazungumzo yao jana jioni hapa Davos ambapo wote wawili wanahudhuria mkutano wa Kiuchumi Duniani wa kila mwaka, maarufu kama World Economic Forum (WEF), ambapo masuala  ya uchumi, athari mbalimbali zinazokabili uchumi duniani kwa sasa na jitihada mbalimbali zinazofanywa kunusuru uchumi huo na njia  za kuleta mabadiliko chanya ya kukuza uchumi barani Afrika yanajadiliwa.

“Afrika inapitia kipindi cha mabadiliko ambayo ni chanya, na Tanzania ni mfano bora wa kuigwa katika hili”. Bw. Cameron amemueleza Rais Kikwete.

Katika mazungumzo yao Rais Kikwete amemueleza Bw. Cameron kuwa kilimo ni sekta kubwa na inayotegemewa na Watanzania wengi na kwamba serikali inalenga  katika kukuza kilimo kwa ajili ya kujitosheleza kwa chakula ndani na nje ya nchi.

Rais Kikwete na Bw. Cameron pia wamezungumzia masuala mbalimbali yanayohusu siasa na usalama barani Afrika.

Mapema jana asubuhi, Rais Kikwete amejumuika na viongozi wengine kutoka Ethiopia, Guinea-Conackry, Kenya na Afrika Kusini  kuzungumzia mabadiliko mbalimbali ya uchumi na maendeleo  barani Afrika.

Katika mjadala huo uliongozwa na Waziri Mkuu wa Zamani wa Uingereza Bw. Gordon Brown, Rais Kikwete amesema pamoja na mabadiliko hayo, bara la Afrika nalo ni sehemu ya Dunia Uchumi, hivyo nayo kupata athari mbalimbali zinazotokana na  mabadiliko hayo ya Kiuchumi duniani.

Rais amesema pamoja na athari na mabadiliko ya Kiuchumi duniani, bado Afrika ina mahitaji zaidi katika kutekeleza sera zinazolenga katika uchumi imara na kuwekeza zaidi katika sekta za elimu, utafiti, kilimo, viwanda na miundombinu.

Rais Kikwete pia amefanya mazungumzo na viongozi na wadau mbalimbali wa maendeleo wakiwemo Bw. Bill Gates, pamoja na viongozi wa Ethiopia na Kenya ambapo wamezungumzia namna ambayo Bw. Gates atatoa mchango wake zaidi katika masuala ya kilimo na utafiti.

Rais Kikwete amekutana na kufanya mazungumzo na Mama Sadako Ogata Rais wa Shirika la Misaada la Japan, maarufu kama Japan  International Cooperation Agency (JICA)  ambaye naye ameelezea kuwa JICA itaendelea kutoa misaada mbalimbali kwa Tanzania pamoja na kwamba yeye amefikia kipindi chakustaafu.

Rais Kikwete pia amekutana na kufanya mazungumzo na  Mkurugenzi Mtendaji wa Vodafone, Bw. Vittorio Colao ambaye ameonesha nia ya kusaidia Tanzania katika kutoa na kusambaza elimu  kwa kutumia simu za mkononi katika masuala mbalimbali ya afya, kilimo na elimu.

Mwisho.

Imetolewa na Premiere Kibanga,
Mwandishi wa Habari Msaidizi wa Rais,
Davos-Switzerland.
27 Januari, 2012

TUCTA YAINGILIA KATI MGOMO WA MADAKTARI!!

Katibu mkuu wa TUCTA, Bw. Nicolas Mgaya,

Shirikisho la vyama vya wafanyakazi nchini Tanzania (TUCTA) limeunga mkono mgomo wa nchi nzima unaofanywa na madaktari na wanataaluma wa afya na kuitaka serikali kushughulikia madai ya madaktari hao sambamba na kushughulikia madai ya wafanyakazi kutoka kada nyingine katika jamii.


Katibu mkuu wa TUCTA, Bw. Nicolas Mgaya, amesema kuwa madai ya wanataaluma wa afya ni sehemu tu ya madai ya muda mrefu yanayotolewa na wafanyakazi nchini na kwamba kuna haja ya serikali kutopuuzia madai hayo.


Wakati Bw. Mgaya akitoa msimamo wa TUCTA, upatikanaji wa huduma za afya katika zahanati na hospitali za umma sehemu mbali mbali nchini, umezidi kuzorota, hasa baada ya kuwepo kwa taarifa kuwa madaktari katika hospitali ya mkoa wa Morogoro nao wamejiunga na mgomo huo.

WAGONJWA WAKOSA HUDUMA KUFUATIA MGOMO WA MADAKTARI MOROGORO!!

Mgomo wa madaktari katika hospitali ya mkoa wa Morogoro umeendelea ambapo baadhi ya wagonjwa waliolazwa katika hospitali wakilalamika kukosa huduma za matibabu huku wakishuhudia vifo kutokea kwa kukosa huduma

Mwandishi wa habari hizi ameshuhudia vyumba vya madaktari vikiwa tupu na huduma za matibabu kutotolewa na kusababisha hali kuwa mbaya zaidi kwa wagonjwa waliolazwa wodini wakiwemo watoto wadogo ambao hawajahudumiwa tangu jana huku baadhi wakikiri kushuhudia  vifo  vya wagonjwa kwa kukosa huduma na baadhi wakitaka waruhusiwe kwenda hospitali binafsi kupata matibabu.

Kwa upande wa wagonjwa wa nje waliokuwa kwenye foleni kutoka wilayani ambao matibabu yao yalishindikana huko wilayani na kulazimika kuhamishishwa katika hospitali ya  mkoa wa Morogoro wamelalamikia kukosa huduma kutwa nzima na hawajui hatma ya matibabu yao.